Karibu RFSU

Publicerad 1/22/2010 | Uppdaterad 10/12/2010

RFSU ni chama kinacho jishughulisha na masuala ya ujinsia hapa Sweden. Chama hiki kiliundwa mwaka 1933 na leo hii ndicho chama kinachoongoza katika kushughulikia masuala ya haki na afya ya ujinsia na uzazi.

RFSU inaamini uwazi katika masuala ya ujinsia kama njia ya kukinga na kuboresha afya. Haki ya kupata elimu na huduma ya afya ya ujinsia na uzazi ni nyenzo muhimu katika kupigania kuwepo jamii yenye afya na usawa. Elimu bora ya ujinsia inawawezesha watu kufurahia ujinsia wao, na pia inampa fursa mtu kufanya maamuzi juu ya mwili wake. Vilevile kuongezeka kwa ufahamu juu ya ujinsia kunazuia mimba zisizotarajiwa, magonjwa yatokanayo na kujamiiana na UKIMWI.

RFSU inatambua aina tatu tofauti za uhuru kama kigezo cha uwezo wa mtu kujithamini na kujiamini: Uhuru wa kuchagua, uhuru wa kufurahia na uhuru wa mtu kujiamulia. Aina hizi za uhuru zinamgusa kila mtu na la muhimu kwa uhuru wa aina hizi ni kuwa, uhuru wa mtu mmoja usisababishe kukosekana kwa uhuru wa mtu mwingine.

RFSU ni shirika lisilo la kiserikali na halina uhusiano wowote wa kisiasa wala dini.

Programu za kimataifa

Kama mmoja wa waanzilishi wa shirikisho la vyama vya uzazi na malezi bora duniani (IPPF), mara zote RFSU imekuwa ikijikita katika masuala ya kimataifa. Dhamira kuu ya shughuli zetu ni kuchangia uboreshaji wa afya ya ujinsia na uzazi kimataifa. Ili kufanikisha azma hiyo, RFSU imekuwa ikitumia uwezo na uzoefu ulioupata kutokana na kujishughulisha na masuala haya kwa miaka sabiini (70). RFSU imebuni njia ya mashirikiano na taasisi mbalimbali ambayo inaweza kuigwa katika mazingira mbalimbali ya kijamii. Shughuli za chama hiki hubuniwa na kutekelezwa kwa kushirikiana na asasi zisizo za kiserikali na wakati mwingine na vyama vya uzazi na malezi bora katika nchi husika. Tunao uzoefu wa kuendesha programu katika nchi kama vile Tanzania, Zambia, Vietnam, Mongolia, China, Urusi, India, Lativia and ndani ya nchi za umoja wa ulaya.

Utetezi

RFSU ina fursa nzuri na ndio inayo ongoza kama mtetezi wa afya ya ujinsia na uzazi na haki zake nchini Sweden na inaitumia fursa hii pekee kwa uangalifu. RFSU inatetea kwa juhudi kubwa kuhusishwa kwa haki za afya ya ujinsia na uzazi katika misaada ya maendeleo itolewayo na nchi ya Sweden na vilevile ile ya Jumuia ya Ulaya. Zaidi ya hapo, tunajitahidi kushawishi ajenda ya haki za ujinsia na uzazi ndani ya mashirika ya kimataifa kama vile Shirika la Afya Duniani (WHO) na Umoja wa Mataifa (UN). Shughuli kubwa tunazofanya katika azma hii ni mikutano isiyo rasmi na wanasiasa, watumishi wa serikali na wale wa mashirika yasiyo ya kiserikali, mikutano iliyo rasmi yenye maudhui maalumu, semina mbalimbali na makongamano. Vilevile tunaandaa ziara za mafunzo kwa wabunge na waandishi wa habari, uelimishaji wa wafanyakazi juu ya haki za afya ya ujinsia na uzazi na kuboresha mtandao wa wafanya maamuzi ambao bado ni vijana nchini Sweden na ndani ya Jumuia ya Ulaya. Ingawa tumejikita zaidi katika masuala ya undeshaji programu, pia tumekuwa wanachama endelevu wa shirikisho la vyama vya uzazi na malezi bora duniani (IPPF) kwa vile tumekuwa tukijitosa katika masuala ambayo ni nyeti kisiasa.

Kliniki ya RFSU

RFSU inaendesha kliniki yake ambayo ndiyo kubwa kulizo zote inayowahudumia vijana nchini Sweden. Pia kliniki hii ni miongoni mwa kliniki chache sana hapa Sweden ambazo watu wenye matatizo yanayohusiana na ujinsia wanaweza kupata ushauri na tiba. Zaidi na hayo, kliniki hii ni mahali pazuri pa kujifunzia mbinu mpya za kushughulikia matatizo yatokanayo na ujinsia.

Kliniki hii ina huduma kuu tatu

  • Huduma za kuzuia mimba, magonjwa yatokanayo na kujamiana na utoaji ushauri nasaha.
  • Ushauri nasaha juu ya kujamiana na tiba ya kisaikologia.
  • Huduma kwenye jamii na uelimishaji (ndani na nje ya Sweden).

Programu za mafunzo na uelimishaji

Miongoni mwa masuala muhimu kwa RFSU toka ianzishwe mwaka 1933 ni kuwepo kwa elimu nzuri ya ujinsia mashuleni. Kwa kweli, mtazamo wetu juu ya elimu wa ujinsia mashuleni ulikuwa kichocheo cha kuhakikisha hatimae elimu hii inatolewa kwenye shule zote za Sweden toka mwaka 1956.

Katika ngazi ya kitaifa, RFSU huandaa shughuli za uelimishaji, semina na mikutano yenye maudhui maalum kwa wanachama wake, waelimishaji rika na wana taaluma kutoka taasisi za tiba na elimu.

RFSU imekuwa ikiandaa mafunzo ya kimataifa toka mwaka 1999. Lengo la mafunzo haya ni kuendeleza masuala ya ujinsia na afya ya uzazi na haki za vijana katika uandaaji wa sera na programu za kijamii na pia kuleta madiliko katika mazingira ya kisera. Programu hii inachangia kuboresha mtandao wa utendaji kazi ndani ya mataifa, nchi na mipaka ya kitaaluma. Washiriki toka nchi na taaluma mbalimbali hupata fursa ya kujadili namna ya kushirikiana katika kazi zinazohusu vijana.

Matawi na wanachama

RFSU inayo matawi 14 yaliyosambaa nchi nzima. Miongoni mwa hayo yapo yaliyo madogo ila wanachama wake ni wenye kujituma, na mengine ni asasi kubwa zenye waajiriwa wake. Matawi hujishughulisha zaidi na uelimishaji rika na elimu ya ujinsia mashuleni. Shughuli zao nyingine ni semina juu ya haki ya afya ya ujinsia na uzazi, kuonyesha filamu, mijadala, utetezi unaowalenga wabunge na vyombo vya habari na pia hugawa kondomu za bure na kuzungumzia juu ya afya ya ujinsia na uzazi na kinga.

Kampuni zetu

RFSU inamiliki kampuni ijulikanayo kama RFSU Inc. Pia RFSU ina hisa zifikiazo 40% katika moja ya kampuni yake ya zamani iitwayo Etac Inc. Nyongeza ya mapato toka kampuni hizi hupelekwa kusaidia huduma zitolewazo na RFSU ambazo haziingizi faida kwa chama. Hizi ni kama vile uelimishaji, tafiti na programu nyinginezo.

Kampuni ya RFSU Inc hutoa kondomu na vitendea kazi vya kiujinsia. Bidhaa za RFSU Inc zinaongoza katika soko la Sweden, Norway, Denmark, na Finland likiwa na asilimia sabiini na tano (75%) ya hisa za soko katika nchi hizo za ki Nordic.

Kampuni yetu ya Etac Inc hubuni, hutengeneza na kuuza vijaa vya kuwasaidia watu wenye udhaifu katika kutembea. Zana hizo ni kama vile magongo ya kutembelea, viti vyenye magurudumu na nyenzo za usafi. Kwa taarifa zaidi tembelea tovuti (ya kiingereza) www.etac.se.

Kwa taarifa zaidi

Ili kufahamu zaidi kuhusu RFSU, tafadhali tembelea tovuti yetu ya kiingereza.

Hitta rätt